Luke 5:1-11

Kuitwa Kwa Wanafunzi Wa Kwanza

(Mathayo 4:18-22; Marko 1:16-20)

1 aSiku moja Yesu alipokuwa amesimama karibu na Ziwa la Genesareti,
Yaani Bahari ya Galilaya.
watu wengi wakiwa wanasongana kumzunguka ili wapate kusikia neno la Mungu,
2akaona mashua mbili ukingoni mwa ziwa, zikiwa zimeachwa hapo na wavuvi waliokuwa wanaosha nyavu zao. 3 cAkaingia katika mojawapo ya hizo mashua ambayo ilikuwa ya Simoni, akamwomba aisogeze ndani ya maji kidogo kutoka ufuoni. Kisha akaketi na kufundisha watu akiwa mle ndani ya mashua.

4 dAlipomaliza kunena, akamwambia Simoni, “Sasa peleka mashua hadi kilindini kisha mshushe nyavu zenu mkavue samaki.”

5 eSimoni akamjibu, “Bwana, tumefanya kazi ya kuchosha usiku kucha na hatukuvua chochote. Lakini, kwa neno lako nitazishusha nyavu.”

6 fNao walipozishusha nyavu zao, wakavua samaki wengi sana, nyavu zao zikajaa zikaanza kukatika. 7Wakawaashiria wavuvi wenzao kwenye ile mashua nyingine ili waje kuwasaidia. Wakaja, wakajaza mashua zote mbili samaki hata zikaanza kuzama.

8 gSimoni Petro alipoona haya yaliyotukia, alianguka miguuni mwa Yesu na kumwambia, “Bwana, ondoka kwangu. Mimi ni mtu mwenye dhambi!” 9Kwa kuwa yeye na wavuvi wenzake walikuwa wameshangazwa sana na wingi wa samaki waliokuwa wamepata. 10 hVivyo hivyo wenzake Simoni, yaani Yakobo na Yohana, wana wa Zebedayo, walishangazwa pia.

Ndipo Yesu akamwambia Simoni, “Usiogope, tangu sasa utakuwa mvuvi wa watu.”
11 iHivyo wakasogeza mashua zao mpaka ufuoni mwa bahari, wakaacha kila kitu na kumfuata.

Copyright information for SwhNEN